Category: Historia

Maji-Maji-warriors-1

Historia ya Vita vya Majimaji inaonesha kuwa awali walikamatwa machifu 48 na baadaye kukamatwa wengine ambapo idadi ya machifu walionyongwa na kuzikwa katika kaburi moja ilifikia 66.

Makumbusho ya Taifa ya Majimaji ni eneo ambalo limehifadhiwa vizuri na serikali ili kuwawezesha watu kujifunza kumbukumbu nyingi ambazo ni kivutio adimu cha utalii wa kishujaa na kiutamaduni.

Watu kutoka mkoa wa Ruvuma na nje ya nchi wanatembelea eneo hili maarufu katika historia ya Tanzania hasa katika harakati ambazo zilifanywa na babu zetu kupambana na wakoloni ili kujitawala wenyewe bila kunyonywa.

Mkurugenzi wa makumbusho ya Taifa ya Majimaji mhifadhi Kiongozi Balthazar Nyamusya anasema eneo hilo la makumbusho lina historia tatu ambazo ni historia ya vita vya majimaji,historia ya ujio wa wangoni kutoka Afrika ya Kusini na historia ya uhuru wa Tanganyika.

Anaitaja historia ya vita vya majimaji ililenga kumkomboa mtanzania kutoka mikononi mwa wakoloni Wajerumani na kwamba sio sahihi kuwa vita hiyo ilikuwa na uwezo wa kugeuza risasi kuwa maji bali ililenga kuwapa nguvu wapiganaji kujitolea hata ikibidi kupoteza maisha ili kujikomboa.

“vita vya majimaji vilianza mwaka 1905 na ilianzia Kilwa na sio Songea, ingawa vita hiyo ilipiganwa katika kanda ya kusini lakini Songea inazungumziwa zaidi kwa sababu watu wote waliokamatwa walinyongwa na kuzikwa Songea katika kaburi moja la pamoja ambalo walizikwa watu 68’’,anasema Nyamusya.

Historia ya Vita vya Majimaji inaonesha kuwa awali walikamatwa machifu 48 na baadaye kukamatwa wengine ambapo idadi ya machifu walionyongwa na kuzikwa katika kaburi moja ilifikia 66.

Unyongaji wa mashujaa hao ulifanyika Februari 27 mwaka 1906, Machi 20,1906 na Aprili 12,1906 katika eneo la Songea club mjini Songea pamoja na eneo la Mahenge mashujaa ambapo walizikwa kaburi moja.

“Siku ya kuwanyonga mashujaa hao watu wengine walikusanyika wakasimamishwa mahali ambapo waliweza kuwaona wanyongwaji ili waone eti wasiige na wao kwa kuwa watanyongwa”,alisema Samwel Gama Mwenyekiti wa Baraza la wazee Makumbusho ya Taifa ya Majimaji.

Gama anabainisha zaidi kuwa wanyongwaji waliletwa katika eneo hilo wakiwa wamefungwa kila mmoja mnyororo mdogo uliofungwa kwenye mnyororo mkubwa na kwamba katika eneo hilo nguzo kubwa mbili zilisimikwa pande mbili.

Anasema juu ya nguzo hizo kulipigiliwa nguzo imara iliyofungwa vitanzi vinne ambapo chini ya nguzo hizo kulikuwa na ubao uliowekwa juu ya nguzo fupi nne.

“Basi waliwafunga wafungwa wanne toka mnyororo ule mkubwa na wakawasimamisha juu ya ule ubao uliotegeshwa,wakawapachika zile kamba zilizoning’inia,kila mmoja na kamba yake huku wakiwa wamefungwa kamba mikono yote miwili ili wasiweze kujimudu na nyuso zao zilikuwa zimefungwa vitambaa vyekundu ili wasiweze kuona”,anasisitiza Gama.

Ili kuwasitiri Gama anasema wanyongwaji hao walifungwa shuka ndogo ili kusitiri uchi wao na kuongeza kuwa askari alifyatua ubao na ndipo miili ya mashujaa hao ikwa inaning’nia kwenye vitanzi mpaka wakakata roho.

“Baada ya mashujaa hao kukata roho katika mateso makali wauaji hao waliiondoa miili hiyo na kuiweka kando katika sehemu hiyo waliowanyongea na kwamba waliwanyonga watu wanne kwa wakati mmoja na kufanya siku ya kwanza yaani Februari 27,1906 kunyonga watu 40”,anaeleza Gama.

Hata hivyo anasema mashujaa walionyongwa vitanzini walikuwa 68,waliokufa gerezani kabla ya kunyongwa walikuwa wawili,waliopigwa risasi kuonesha nguvu ya risasi walikuwa watano na kufanya jumla mashujaa 75 kuuawa kikatili.

Kulingana na Mwenyekiti huyo wa Baraza la wazee,kaburi kubwa lililochimbwa na wafungwa kwa mwezi mmoja katika eneo la mashujaa mjini Songea ambalo limetengwa eneo la kumbukumbu ya mashujaa wa vita vya majimaji.

“maiti ya mashujaa walionyongwa kwa siku moja ililazwa katika kaburi hilo kiubavu bila sanda na kufukiwa kidogo ili kutoa nafasi kwa maiti wengine siku nyingine ili waje kulazwa juu ya wale wa kwanza na kufikia tena kidogo mpaka wote walionyongwa watakapozikwa katika kaburi moja kubwa’’,anasema Gama.

Hata hivyo anasema chifu wa wangoni yaani Nduna Songea Mbano hakuzikwa katika kaburi moja na wenzake kwa kuwa yeye aliuawa siku ya peke yake tarehe 4/3/1906 baada ya wengine wote kunyongwa.

Anasema chifu Songea Mbano alikuwa ndiyo Jemedari Mkuu wa Jeshi la wangoni na alikuwa ni hodari sana asiyeogopa lolote kwa hiyo wajerumani walitaka abakie ili wamtumie kwa malengo yao.

“Chifu Songea alidai na yeye anyongwe kama walivyonyongwa ndugu zake,basi alinyongwa na wajerumani waliondoka na kichwa chake wakakiweka ndani ya kasha na kuondoka nacho kwenda Ujerumani ambako hakijarudi hadi leo”,anadai Gama.

Anabainisha kuwa mwili wa chifu Songea Mbano ukiwa kiwiliwili bila kichwa ulizikwa katika kaburi la pekee yake katika eneo la mashujaa la mjini Songea na kuongeza kuwa mashujaa wote hao walionyongwa na kuzikwa walikuwa na imani zao mbalimbali za kidini.

Mhifadhi Kiongozi wa Makumbusho ya Taifa Philipo Maligisu anasema kuwa katika makumbusho ya Taifa ya Majimaji zimewekwa kumbukumbu zote muhimu za historia ya majimaji ambapo watu wengi kutoka ndani na nje ya nchi wanafika kuangalia makumbusho haya ambayo yamekuwa ni kivutio kikubwa cha utalii.

Historia inaonesha kuwa Songea ndiyo ilikuwa sehemu ya kwanza ya kupima uwezo wa dawa ya Majimaji kabla ya kwenda katika maeneo mengine ya kusini ambako vita hiyo ilipiganwa.

Hata hivyo anasema vita hiyo ilianza kupigwa katika eneo la Kilwa Kivinje wilaya ya Utete ikiongozwa na Kinjekitile na wenzake na walifanikiwa kuchoma boma za wajerumani baada ya kwenda huko usiku na sio mchana.

“Dawa ya majimaji iliaminika kuwa inafaa baada ya kujaribiwa katika eneo la Songea na wajumbe wote waliokuwa wanakwenda kuchukua ile dawa waliliridhika na ubora wa dawa ambapo Kinjekitile Ngwale alikuwa ni mwanzilishi wa dawa hiyo pamoja na vita yenyewe ya majimaji’’,anasema Maligisu mhifadhi kiongozi wa makumbusho ya Taifa.

Katika makumbusho ya Taifa ya majimaji kuna kumbukumbu ya silaha mbalimbali walizotumia mashujaa wa majimaji kupigana na mkoloni ukiwemo mkuki ambao ulipatikana nyumbani kwa chief Songea Mbano wa kabila la wangoni ambaye alikuwa anautumia mwenyewe katika mapigano.

Makumbusho hayo pia yana vitu mbalimbali vya kale vikiwemo mafiga ya mawe, kiko, majembe ya kale pia kuna chungu kikubwa alichokuwa anatumia chifu Songea Mbano ambacho kilikuwa kinatumika kuhifadhia mazao kama vile karanga ambacho kilifukiwa mwaka 1905.

Chungu hicho kiligundulika mwaka 1980 katika eneo la Mputa wilayani Namtumbo ambapo mtu mmoja wakati analima shamba lake alikigonga chungu hicho na alipoangalia akakuta karanga nyingi na inaaminika chungu hicho alikuwa anatumia mke wa chifu Mputa wa Songea.

Read More
PICHA MOJA

Fahamu Historia ya Mji wa Songea, ulionzishwa mwaka 1897

Muonekano wa mji wa Songea mwaka 1897
Mashujaa 67 wa vita ya Majimaji ambao walinyongwa na wajerumani mwaka 1906 kisha kuzikwa ndani ya makumbuisho ya Taifa ya Majimaji ambako kuna makaburi mawili,kaburi kubwa ni la mashujaa 66 ambao wamezikwa pamoja na kaburi moja ni la Jemedari wa wangoni Nduna Songea Mbano
Jemedari wa Kabila la wangoni Nduna Songea  Mbano ambaye jina lake limepewa mji wa Songea,picha hiyo alipigwa na wajerumani mwaka 1906 muda mfupi kabla ya kunyongwa na wajerumani
Mnara ambao umejengwa katika eneo la Songea Club mahali ambapo walinyongwa kikatili na wajerumani mashujaa 67 mwaka 1906 kisha kwentda kuzikwa ndani ya makumbusho ya Majimaji Mahenge Songea
Katikati ni Chifu wa Tano wa Kabila la wangoni Nduna Imanuel Zulu Mbano akiwa ndani ya Makumbusho ya Taifa ya Majimaji mjini Songea

MJI wa Songea uliopo katika Mkoa wa Ruvuma  ni miongoni mwa maeneo machache hapa nchini ambayo yana hazina kubwa ya utajiri  wa kihistoria  na kishujaa.

Mashujaa kutoka katika Mji wa Songea waliendeleza mapambano dhidi ya ukoloni wa Kijerumani hivyo kuchangia kikamilifu harakati za ukombozi kabla ya kupata uhuru wa Tanganyika mwaka 1961.

Jina la Mji wa Songea ni kumbukumbu ya Nduna Songea Mbano ambaye alikuwa na Ikulu yake katika Mji wa Songea. Mji wa Songea una majengo ya kumbukumbu za kihistoria mbalimbali yakiwemo makanisa yenye miaka zaidi ya 100.

Mhifadhi Kiongozi wa Makumbusho ya Taifa ya Majimaji Bartazar Nyamusya anasema historia inaonesha kuwa Mji wa Songea ulianzishwa mwaka 1897 kama kituo cha kijeshi cha Kijerumani.

Hata hivyo anasema Mji wa Songea uliendelea kukua na kuwa Makao makuu ya utawala wa Wajerumani katika Wilaya ya Songe ana kwamba Mji huo ulizinduliwa rasmi kuwa mji wa kihistoria, kishujaa na kiutalii mwaka 2010.

Historia inaonesha kuwa Mji wa Songea  uliathirika na Vita ya Majimaji kati ya mwaka 1905 hadi 1907 na Vita kuu ya pili ya Dunia kati ya mwaka 1939 hadi 1945.

Licha ya Mji huo kuathirika na vita hivyo,Nyamusya anasema mji uliendelea kuwa Makao makuu ya Mkoa wa Ruvuma wakati wa utawala wa  Waingereza katika Tanganyika, baada ya uhuru hadi leo  bado Songea ndiyo Makao Makuu ya Mkoa wa Ruvuma.

 Mji wa Songea una umaarufu wa mashujaa wa Vita ya Majimaji ambapo mashujaa 67 walinyongwa mwaka 1906 kati yao mashujaa 66 walizikwa katika kaburi moja.

Nduna Songea Mbano ambaye alikuwa na umaarufu, alinyongwa na  kuzikwa katika kaburi lake  ambapo makaburi yote yapo katika Makumbusho ya Taifa ya Majimaji Songea.

Mashujaa hao 67 walinyongwa katika eneo lililojengwa Mnara wa Mashujaa wa vita ya Majimaji nyuma ya ukumbi wa Songea ambalo ni kivutio cha aina yake cha utalii katika Mji wa Songea.

Mkoa wa Ruvuma pia ulitoa mashujaa walioshiriki katika Vita kuu ya pili ya Dunia ambapo mashujaa 270 walishiriki katika vita hiyo kati yao mashujaa watatu walikuwa ni wanawake. 

Makumbusho ya Majimaji yalianzishwa rasmi mwaka 1980 na kusimamiwa na Hayati Dk.Lawrence Gama wakati huo alikuwa Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma.

Mchakato wa kuyakabidhi Makumbusho hayo chini ya Shirika la Makumbusho ya Taifa ulianza Mei hadi Novemba 2009 ukisimamiwa na aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Dk.Christine Ishengoma.

Makumbusho hayo yalikabidhiwa katika Shirika la Makumbusho ya Taifa chini ya sheria ya makumbusho ya Taifa la Tanzania, namba saba ya mwaka 1980 hivyo makumbusho hayo yalipandishwa hadhi na kuwa Makumbusho ya Taifa mwaka 2010.

Haya ni Makumbusho pekee nchini ambayo imebahatika kuwa na vifaa muhimu katika historia ya Mtanzania, mchakato uliopo hivi sasa ni Makumbusho hayo kuchukuliwa kuwa ya Kitaifa chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii ili iwe endelevu.

Mji wa Songea ni miongoni mwa miji michache ambayo ilitoa upinzani mkali katika vita vya Majimaji ambapo katika Makumbusho hayo kuna ushahidi ambao unaonesha moja kwa moja kuwa wazee wa Songea walishiriki kikamilifu katika vita hiyo.

Makumbusho haya yaliitwa Makumbusho ya Mashujaa wa vita ya Majimaji kwa sababu ni eneo ambalo lina makaburi mawili ya mashujaa walionyongwa wakati wa vita ya Majimaji kipindi cha utawala wa Mjerumani.

Ukitazama nje ya Makumbusho hayo kuna sanamu za wapiganaji wa vita ya Majimaji.Majina ya sanamu za wapigaji hao ambao waliwahi kutawala Songea ni Mpambalyoto Soko bin Msarawani na Nduna Songea Mbano bin Luwafu.

Majina mengine ni Nduna Chabruma Gama bin Hawayi, Zimamoto Gama bin Fusi, Nkosi Mputa Gama bin Gwazerepasi, Nduna Zamchaya Gama bin Gwazerepasi, Mtepa Ntara bin Kanyoka na Nduna Usangira Gama bin Mheshimiwa Waarule.

Wapiganaji wengine ni Magodi Mbano bin Mbamba, Njorosa Mbano bin Mbamba, Masese Parangu Mbano bin Songea, Nyunyusea Mbano bin Njenje na Njorosa Mbano bin MbambaUrithi huu wa utamaduni uliopo katika Makumbusho ya Taifa. 

Majimaji ni hazina kubwa ya vivutio vya utalii wa kihistoria na kiutamaduni ambaoiendelezwa unaweza kuingiza pato kwa wakazi wa Mkoa wa Ruvuma.

Makumbusho ya Taifa ya Majimaji yana malikale ambazo zimehifadhiwa na zinaweza kutumika kama kivutio cha utalii na kujifunza historia ya mashujaa na urithi ambao unapatikana katika Mkoa wa Ruvuma.

Tanzania ina nyumba kadhaa za Makumbusho ya Taifa katika maeneo mbalimbali nchini ambazo Makumbusho na Nyumba ya Utamaduni Dar es salaam, Kijiji cha Makumbusho ya Taifa Dar es Salaam, Makumbusho ya Elimu Viumbe Arusha, Makumbusho ya Azimio la Arusha, Makumbusho ya Mwalimu Julius Nyerere Butiama na  Makumbusho ya Taifa ya Majimaji Songea.

Read More